Maabara


Upimaji wa Magonjwa Yanayoambukizwa kwa njia ya damu (TTIs): 

Mpango wa Taifa wa Damu Salama una maabara ambazo ziko katika vituo vya Kanda vinavyofanya uchunguzi wa kimaabara wa damu baada ya kuwa imekusanywa kutoka kwa wachangiaji. Kwa ujumla upimaji wa damu wa kimaabara umewekwa katika maabara hizi zilizoko katika kanda nane (8) zilizowekwa kimkakati tofauti na ukusanyaji wa damu ambao umegatuliwa hadi ngazi ya Halmashauri. Kanda hizi ni Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam), Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro), Kanda ya Kusini (Mtwara), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Magharibi (Tabora), Kanda ya Ziwa (Mwanza) na Kanda ya Jeshi (Lugalo).                    

Kila chupa ya damu  hupimwa  Virusi vya UKIMWI (VVU), Virusi vya Hpoma ya Ini B (HBV), Virusi vya Homa ya Ini C (HCV), na Kaswende kwa kutumia teknolojia ya Chemiluminescent Microparticle Immunoassay (CMIA) ambayo ni teknolojia ya kisasa  kabisa na mahsusi yenye uwezo mkubwa wa kubaini maambukizi ya magonjwa.           

 Upimaji wa Makundi ya  Damu: 

Kila chupa ya damu  hupimwa  kundi la damu aina ya ABO na Rh. Vikevile vipimo vya ziada hufanywa kwa ajili kubaini usalama wa damu kwa kuangalia uwepo wa kingamwili zisizotarajiwa (Screening for unexpected antibodies & determination of high titre ABO antibodies in plasma). 

Uzalishaji wa Mazao ya Damu         

 Mpango wa Taifa wa Damu Salama huchakata damu zinazokusanywa kutoka kwa wachangiaji kuwa mazao ya damu kama vile chembechembe hai nyekundu za damu, majimaji ya damu (Plasma), chembe sahani (Platelets) na  cryoprecipitate. Aidha Mpoango huchakata mazao ya damu kwaajili ya wagonjwa wenye mahitaji maalum (hasa wanaopandikizwa viungo) kwa kutumia teknolojia ya kupunguza seli hai nyeupe (leucoreduction) au kwa kutumia miale (irradiation).     

Uhifadhi wa Damu na Mazao ya Damu:       

Mpango wa Taifa wa Damu Salama una vifaa kwa ajili ya kuhifadhi wa damu na mazao ya  damu katika jotoridi linalofaa kulingana na aina ya mazao ya damu. Vifaa vya mnyororo baridi  vilivyowekwa katika maabara za Mpango ni pamoja na vyumba vya baridi (cold rooms), majokofu, incubators kwa ajili ya uhifadhi wa chembe sahani (platelet). Halijoto kwenye vifaa hivi vya kuhifadhi hufuatiliwa kiotomatiki kwa kutumia vifaa vya kielektroniki ambavyo hutoa tahadhari kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka halijoto inapotoka nje ya kiwango kilichokusudiwa              

Ugavi  wa Damu Salama     

 Maabara za Damu Salama hugawa  damu salama na mazao ya damu kwa hospitali na vituo vya afya vilivyosajiliwa na kuruhusiwa kutoa huduma ya damu kwa wagonjwa.  Vituo vya kutolewa huduma za damu salama  huomba damu na mazao ya damu  kwa kujaza fomu za maombi ya damu. Fomu hizo huwasilishwa kwa maabara za Damu Salama  ambazo hukagua maombi na kutoa mazao ya damu  yaliyoombwa  kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki  wa ugavi wa damu salama.