Kwanini uchangie damu


Mahitaji ya damu yanakadiriwa kuwa asilimia moja (1%) ya jumla wananchi  kulingana na ushauri wa Shirika la Afya Duniani (WHO) . Kwahiyo mahitaji ya damu nchini yanakadiriwa kuwa chupa za damu  550,000 kwa mwaka wa  2022/2023 kulingana na makadirio ya sensa ya 2012. Idadi ya sasa ya chupa za damu zinazokusanywa kwa mwaka iko chini ya makadirio haya kwani makusanyo ya mwaka ya 2020/2021 yalikuwa chupa za damu 330,000. Takwimu zinaonesha wazi mahitaji ya damu ambayo hayajafikiwa nchini. Kwa hivyo, Mpango wa Damu Salama  unawasihi watu wote kote nchini wenye sifa za  kuchangia damu kuchangia damu ili kufidia pengo la asilimia 40 ya mahitaji ya damu nchini.            

Kuchangia damu ni tendo la hisani kwani huokoa maisha ya wale wanaohitaji. Mpango wa Taifa wa Damu Salama huhamasisha uchangiaji wa hiari wa damu kauli mbiu maarufu inayosema "Changa Damu, Okoa Maisha"                                             

Matumizi ya damu nchini ni makubwa baina ya makundi yafuatayo ya wagonjwa; akina mama wajawazito wanaopoteza damu wakati wa kujifungua, watoto wenye umri chini ya miaka 5, wahanga wa ajali za barabarani na wagonjwa wa saratani. Hivyo kila mwananchi mwenye afya njema anasisitizwa kuchangia damu ili kuhakikisha akiba  ya damu inadumishwa ili kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji hasa katika kuunga mkono ajenda ya kupunguza vifo vya wajawazito nchini Tanzania.