HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA NCHINI ZAANZA KUZALISHA MAZAO YA DAMU
Posted on: December 4th, 2022Na. Catherine Sungura, WAF,Dar Es Salaam
Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa kuanza kuzalisha mazao ya damu ili kuimarisha huduma za damu salama nchini.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Meneja Mpango wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama Dkt. Abdu Juma Bhombo wakati akiongea na Waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam kuelekea uzinduzi wa Kampeni ya uhamasishaji na uchangiaji wa damu salama kwa kushirikiana na Redio ya UFM chini ya Azama Media Group.
Dkt. Juma amesema hivi sasa Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama imeanza utekelezaji wa kuongeza wigo wa utengenezaji wa mazao damu kwa kuhusisha Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda tofauti na hapo awali ambapo uzalishaji huu ulikuwa ukifanyika katika vituo vya Damu Salama-Kanda.
Amesema hadi sasa hospitali ambazo zimeshajengewa uwezo wa kutengeneza mazao ya damu ni Hospitali ya Mkoa wa Geita, Simiyu, Iringa, Arusha-Mount Meru, Hospitali ya Mloganzila, Benjamin Mkapa, Taasisi ya Mifupa-MOI, CCBRT, na Hospitali ya Taifa Muhimbili uzalishaji ni wa moja kwa moja wakati mtu anapochangia damu kulingana na mahitaji ya kituo.
Aidha, Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeanzisha uchangiaji wa damu kwa njia ya 'Apheresis' ambapo mchangia damu anaweza kuchangia aina fulani ya mazao ya damu yanayohitajika.
"Hii ni teknolojia mpya na itawezesha upatikanaji wa mazao ya damu yenye viwango na ubora na yataongeza ufanisi wa matibabu kwa wagonjwa wanaoongezewa damu hasa wagonjwa wa saratani".
"Mafanikio haya yanatokana na uwezeshaji wa Serikali ya Awamu ya Sita hasa katika ununuzi wa kununua mashine za kisasa za 'apheresis' na vifaa tiba vingine vya kutengenezea mazao ya damu. "Amesema Dkt. Juma
Aidha, amesema mahitaji ya sasa ya yamefikia asilimia 76 ambapo Wizara ya Afya imeweka malengo ya kukusanya chupa 550,000 za damu ambayo ndio mahitaji ya nchi kwa Mwaka.
Kwa upande wa mashirikiano hayo Dkt. Juma amesema Kituo cha Radio UFM FM na Kampuni na AM Creative watafanya uhamasishaji kwa jamii wakati wa ratiba za uhamasishaji uchangiaji damu salama katika sherehe za Serikali za Kitaifa Nchi nzima kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Iringa.
Naye, Mhariri Mkuu wa Radio UFM FM Bw. Ramadhani Tuwa amesema wameamua kuhamasisha uchangiaji damu salama kupitia Radio yao kwani wamekuwa wakiripoti matukio mengi yenye uhitaji wa damu hivyo wameona vyema kushirikiana Serikali kutoa elimu.