MPANGO WA DAMU SALAMA WATAKIWA KUONGEZA USIMAMIZI UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: June 28th, 2022

Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini umetakiwa kuongeza juhudi katika kusimamia na kuratibu kazi zote zinazofanywa katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya Mikoa na halmashauri katika viwango vinavyokusudiwa ili viweze kupata utambuzi rasmi.

Hayo yamebainishwa na Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Saitole Laizer Mkoani Morogoro katika hafla fupi ya kukabidhi vyeti vya Ithibati kwa vituo sita vya kanda za Mpango wa Taifa wa Damu Salama na Mpango wa Taifa wa Damu salama Zanzibar ambapo amesema kuwa Tanzania inakuwa nchi ya tatu kupata Ithibati ya hatua ya tatu ya kuwa na vituo sita vya damu salama nchini vyenye utambuzi rasmi.

“Tanzania inaweza kuruhusiwa kuuza mazao ya Damu Salama mahali popote duniani kwani tumefikia viwango vya ubora vinavyokubalika kimataifa”, amesema Dkt Laizer.

Dkt. Laizer amesema chombo kinachotoa idhibati hiyo ni chombo cha kimataifa kinachoitwa Afrika Association of Blood Transfusion ambapo taasisi hiyo inapita kila nchi na kutizama ubora wa huduma ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama.

Dkt.Laizer metoa wito kwa Mpango wa Taifa wa Damu Salama nchini kuendelea kuhakikisha kwamba ubora wa Huduma uliopatikana katika hali ya juu bila kuteteleka.

“Maana kufikia kiwango cha juu ni hatua moja lakini kuendelea kubaki kiwango cha juu pia ni hatua nyingine”, amesema Dkt.Laizer

Dkt. Laizer amesisitiza Mpango wa Taifa wa Damu Salama Nchini kutatua changamoto zilizopo kuhakikisha wanalinda ubora walioupata na kwamba serikali iko bega kwa bega na kuona Mpango huo unakwenda kuwa endelevu na kuboreka kila mwaka.

Vituo sita vilivyopata ithibati hiyo ni Kanda ya Kaskazini Mkoa wa Kilimanjaro, Kanda ya Ziwa- Mwanza, Kanda ya nyanda za Juu Kusini- Mbeya, Kanda ya Magharibi- Tabora, Kanda ya Kusini- Mtwara pamoja na Mpango wa Taifa wa Damu Salama Zanzibar.