Jamii msiwe na hofu ya kuchangia damu wakati huu wa COVID-19, bado tunahitaji kuokoa maisha -Dkt Kitundya

Posted on: November 17th, 2020

Kitengo cha damu salama katika hospitali ya rufaa mkoa wa Dodoma nchini Tanzania kimewatoa hofu wachangiaji wa damu kuwa uwepo wa ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 usiwatishe kwenda kuchangia damu kwani hawawezi kuambukizwa wala kuwaambukiza wengine kwa kuchangia damu. 

Msimamizi  wa kitengo hicho Dkt. Leah Kitundya anasema kwa sasa kiwango cha uchangiaji wa damu kimepungua kwa sababu wachangiaji wakubwa ni wanafunzi wa sekondari na vyuo ambao wamerudi nyumbani baada ya masomo kusitishwa  kwa lengo la kuepuka msongamano  unaoweza kuchangia maambukizi mapya ya virusi hivyo wakishirikiana na wanajeshi.

Dkt.  Leah akaongeza kuwa changamoto ya virusi vya Corona vimeathiri kwa kiasi kikubwa uchangiaji wa damu na kusababisha kutofikia lengo walilojiwekea  la kila mwezi kukusanya chupa 1000 hadi 1500 lakini sasa hali imekuwa tofauti ambapo kwa mwezi uliopita wamekusanya chupa 500 akisema kuwa mwitiko wa wananchi kujitokeza kuchangia ni mdogo.

Amesema kuwa, "jamii haina mwamko wa kuchangia damu, mwezi uliopita tulipata  chupa  za damu 558 kiasi kwamba  tumerudi  nyuma sana. Kipindi cha nyuma kwa mwezi tulikuwa tunakusanya chupa 800 hadi 900 lakini mwezi uliopita tumekusanya chupa 500 tu.  Kwa hivyo tumerudi nyuma sana.Kwa hio sasa basi tukisema hatuchangii damu kwa sababu ya corona tunasema wenzetu ambao wamelala hospitalini wapoteze maisha. Ni nani anayetakiwa kuchangia damu? Ni mimi na wewe ilimradi tu uwe na umri wa kuanzia miaka 18 hadi 65. Uzito kilo 50  kwenda juu,usiwe na magonjwa sugu kama kuanguka kifafa ,magonjwa ya moyo,ugonjwa wa kisukari ugonjwa wa pumu na usiwe mama mnyonyeshaji mtoto wa chini ya miezi sita au mama mwenye hali ya ujauzito." 

Dkt. Leah amesema hata hivyo kuwa wanachukua tahadhari  wakati wa uchangiaji wa damu katiki kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya Corona.

Kuhusu suala ya kwamba ukichangia damu unatapa ugonjwa wa Corona, Dkt. Leah amesema, "lakini kuchangia damu sio eti ile damu yaweza kuambukiza mtu kupata corona apana!  kunafanya kazi tukichukuwa usalama ilikuzuia watu wasipate maambukizi ya Corona."

Pia msimamizi huyo akatoa ufafanuzi juu ya malalamiko ambayo hutolewa na baadhi ya watu kuwa wamekuwa wakitozwa fedha kupata damu kwa ajili ya wagonjwa wao  akisema kuwa, "kulipia sio kulipia kwa  hela uchangiaji wa hiari unakuwa mwanachama na unapata kadi siku ambayo utakuwa mgonjwa unaambiwa hakuna kulipia hiyo damu ya kulipia kwa maana ya kurudisha sio kwa kuchangia hela."

 

Mada: 

Afrika

COVID-19

Coronavirus

Virusi Vya Corona

Damu Salama

Dodoma

Tanzania

Source: 

UN News